SERIKALI IBORESHE MFUMO WA SCADA KUDHIBITI UPOTEVU WA MAFUTA-KAMATI YA BUNGENa mwandishi wetu

📌 *Wataka mfumo wa SCADA uwe chini ya Serikali*

📌 *Waagiza flowmeter kuwekewa uzio*


Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imeishauri Serikali kupitia kwa Wakala wa Uagizaji wa Mafuta kwa pamoja (PBPA) kuufanyia maboresho mfumo wa SCADA ambao umebuniwa kwa lengo la kudhibiti changamoto ya upotevu wa Mafuta yanayoingizwa nchini.

Ushauri huo umetolewa na Mwenyejikiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Mhe. Mathayo David Mathayo wakati wa ziara ya kutembelea miundombinu inayotumika kupakua na kuhifadhi mafuta katika bandari ya Dar es Salaam, February 23, 2024.

Mhe. Mathayo amesema kuwa mfumo wa Supervisory Control And Data Acquisition (SCADA) uendelee kufanyiwa maboresho ili lengo la kuanzishwa kwake lifikiwe kama Serikali ilivyokusudia katika masuala ya udhibiti na usalama wa mafuta pamoja na  utunzaji wa kumbukumbu muhimu za mafuta.

"Umiliki wa Mfumo wa SCADA uwe chini ya Serikali mara baada ya mkataba wa mkandarasi aliyefunga mfumo huo kumalizika, sio tena kubakia kwa mkandarasi ili kuweza kuimarisha ulinzi katika mfumo huo." Amesema Mathayo

Kamati imeshauri kuwa flowmeter zote zilizopo Bandari ya Dar es Salaam ziwekewe uzio pamoja na kufunga kamera za kisasa  (CCTV camera) kwa sababu zinasaidia kutazama usalama wa Nchi kwenye masuala ya mafuta ikiwemo udhibiti na ubora wa mafuta.

Amesema kampuni ya Tiper itazame uwezekano wa kupunguza gharama ya kuhifadhi mafuta kwenye matenki yake, jambo litakalosaidia kuwapunguzia gharama wafanyabishara wadogo wanaotumia miundombinu ya Tiper kuhifadhi mafuta yao.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu Wizara ya Nishati Mha. Felchesmi Mramba amesema kuwa maelekezo yote yaliyotolewa na Kamati ya Kudumu ya Bunge yatafanyiwa kazi ipasavyo.


Post a Comment

0 Comments