BoT YATAJA ADHABU WANAOUZA FEDHA ZA KIGENI KIHOLELA

 Na mwandishi wetu

Benki Kuu ya Tanzania imetaja adhabu atakayopata anayeuza fedha za kigeni kinyume na sheria. Adhabu hiyo imetajwa na Gavana wa Benki Kuu, Bw. Emmanuel Tutuba alipokutana na wamiliki na waendeshaji wa hoteli za kitalii jijini Arusha tarehe 23 Machi, 2024.


Gavana Tutuba amesema fedha zozote zinazoingia nchini hazitakiwi kuingia kwenye soko haramu la kuuza fedha za kigeni na yeyote atakayefanya hivyo anaweza kuhukumiwa kifungo cha miaka 14 jela.


“Kwa mamlaka niliyopewa naweza nikakupa adhabu ya kiwango cha dola za Kimarekani 3,000 ambazo zinaweza kulipwa kwa shilingi ya Tanzania. Lakini nikiona haufuati taratibu naweza nikakupeleka mahakamani na unaweza kuhukumiwa kifungo mpaka cha miaka 14 jela,” alisema Gavana Tutuba.


Aidha, aliongeza kuwa dhamira ya Benki Kuu ya Tanzania ni kurahisisha mazingira ya kufanyia biashara kwa lengo la kustawisha sekta hiyo. 


Alisisitiza kuwa BoT inawataka wadau wa sekta ya fedha kufata sheria na miongozo mbalimbali ili kukuza uchumi wa nchi.

“Sisi kama wasimamizi wa sekta hii tunataka kuongeza uzingatiaji wa sheria ila sio kwa kutumia mabavu bali kwa kukutana na ninyi, tuzungumze na tupate suluhu ya changamoto zilizopo, alisema.” 


“Dhamira yetu kama wasimamizi wa Uchumi wa nchi ni kurahisisha mazingira ya kufanyia biashara ili kila mmoja afanye biashara kwa weledi,” aliongeza Gavana Tutuba.


Akijibu hoja ya mmoja wa washiriki, Meneja wa Taasisi Maalum za Fedha, Bi. Suzan Katabi, alisema kuruhusiwa kwa hoteli mkoani humo kupata leseni za kutoa huduma ya kubadilisha fedha za kigeni kutasaidia kupanua wigo wa huduma hiyo kutokana na kwamba mkoa huo una maduka 7 tu ya kubadilisha fedha za kigeni.


Kwa upande wao, washiriki wa mkutano huo waliishukuru Benki Kuu kwa kutambua mchango wao katika kukuza sekta ya utalii ambayo inaongezea nchi fedha za kigeni. Pia, waliishauri BoT kuweka nguvu kubwa kuhakikisha  wageni na wenyeji nchini wanatumia kadi za kuchanja kwenye kufanya malipo.
Post a Comment

0 Comments