DKT. BITEKO ATOA MAAGIZO MANNE UIMARISHAJI HUDUMA ZA AFYA

 OR-TAMISEMI


Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko ametoa maagizo manne likiwemo la kutaka kuwekwa Mpango Mkakati wa kuhakikisha uwekezaji wa miundombinu uliofanywa na Serikali katika vituo ngazi ya Afya ya Msingi inatunzwa. 


Dkt. Biteko ametoa maagizo hayo leo Machi 25, 2024  wakati akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kufungua Mkutano wa Kwanza wa Kimataifa wa Afya ya Msingi. 


Mkutano huo pia umeenda sambamba na uzinduaji wa namba 115 itakayotumiwa kwenye programu ya usafirisaji wa dharura kwa wajawazito waliojifungua na watoro wachanga. 


Amesema wizara zinazoshughulikia sekta ya afya zinapaswa kuweka mikakati ya kutunza miundombinu ambayo inachangia upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi kwa urahisi zaidi.


Dkt. Biteko amewataka kujadili kwa kina namna bora ya kubuni mbinu zitakazowezesha kuongeza kasi ya kuajiri wataalam wa kada mbalimbali za afya hasa zile zenye upungufu mkubwa.


Pia, ameagiza kuainisha mikakati ya utoaji wa elimu ya afya kwa jamii ili wananchi waelimishwe kuhusu njia za kuzuia magonjwa, umuhimu wa chanjo na njia zingine za kudumisha afya bora.


Amesisitiza kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji na tathmini ya huduma za afya ya msingi ili kuweza kufahamu maendeleo ya utekelezaji wa Afua mbalimbali za afya na kutambua maeneo ya kuboresha.


Aidha Dkt. Biteko amesisitiza kuwa Serink imeweza kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kuimarisha miundombinu ya utoaji huduma ambapo kuanzia mwaka 2017 hadi Januari 2024, jumla ya vituo 2,799 vimejengwa na vingine kufanyiwa ukarabati, zikiwemo Zahanati 1,762, Vituo vya Afya 910, na Hospitali za Halmashauri 127.


Pia, majengo 83 ya kutolea huduma za dharura na majengo 28 kwa ajili ya wagonjwa mahututi na nyumba za watumishi 150  zimejengwa. Gharama ya ujenzi na ukarabati huo imefikia shilingi bilioni 937.2 ikiwa ni hatua muhimu katika kuhakikisha kuwa huduma za afya zinapatikana.


Post a Comment

0 Comments