KIPINDI CHA MIAKA 60 YA MUUNGANO WA TANGANYIKA NA ZANZIBAR UTATUZI WA HOJA ZA MUUNGANO UMEIMARIKA-WAZIRI JAFO

 Na mwandishi wetu,Dodoma

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo amesema kuwa katika kipindi cha katika kipindi cha miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar utatuzi wa hoja za Muungano umeendelea kuimarika.


Kutokana na hali hiyo, amewaasa wananchi kuulinda na kuenzi Muungano akisema kuwa ni wa kipekee barani Afrika na duniani kote akisisitiza kuwa umekuwa ni wa faida nyingi zinazoufanya uendelee kuimarika.


Amesema Serikali zote mbili zimeweka Mwongozo rasmi wa vikao vya Kamati ya Pamoja ya Kushughulikia Masuala ya Muungano ambavyo hushirikisha wajumbe kutoka pande zote mbili za Muungano ambavyo hufanyika katika ngazi za Makatibu Wakuu, Mawaziri na kikao cha Kamati ya Pamoja ambacho Mwenyekiti wake ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. 


Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, jijini Dodoma leo  Machi 26, 2024, Dodoma, Dkt. Jafo amesema tangu kuanzishwa kwa utaratibu wa vikao vya pamoja mwaka 2006, hoja 22 zimepatiwa ufumbuzi kati ya hoja 25 zilizoibuliwa.


Amesema hoja nyingi ambazo zilikuwa hazijapatiwa ufumbuzi zimejadiliwa na pande zote mbili za Muungano na kupatiwa ufumbuzi ambapo katika kipindi cha mwaka 2021 hadi 2024 pekee hoja 15 zimepatiwa ufumbuzi kati ya hoja 18 zilizokuwepo kwa kipindi hicho. Hoja zilizobakia zipo katika hatua mbalimbali za kupatiwa ufumbuzi.


Waziri Jafo amesisitiza katika kuhakikisha usawa wa utoaji wa huduma kwa wananchi wa pande zote mbili za Muungano, Taasisi za Muungano zilizopo Tanzania Bara zimefungua Ofisi Zanzibar ambapo hadi sasa Taasisi 33 zimefungua Ofisi Zanzibar kati ya Taasisi 37 za Muungano.

Kwa upande wa Mazingira amesema kuwa Serikali imeendelea kutekeleza Sera ya Taifa ya Mazingira ya mwaka 1997 na baadaye Sera ya Mazingira ya mwaka 2021 ambapo mafanikio makubwa yamepatikana katika uhifadhi na usimamizi wa mazingira ikiwa ni pamoja na kuratibu utekelezaji wa Kampeni ya Upandaji Miti nchini ambapo kila Halmashauri ya Wilaya imeelekezwa kupanda miti milioni 1.5 kila mwaka.


Post a Comment

0 Comments