LAAC YACHUKIZWA KUTOFWATWA KWA MIONGOZO KATIKA KUTEKELEZWA MIRADI YA ELIMU NA AFYA

 Na Angela Msimbira,. BUTIAMA


Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za  Serikali Mitaa(LAAC) imeonesha kukerwa na hatua ya Halmashauri ya Wilaya ya Butiama mkoani Mara kushindwa kufuata miongozo ya utekelezaji wa miradi ya afya na elimu. 


Akizungumza leo Machi 25, 2024 wakati wa ziara ya ukaguzi ujezi wa shule mpya ya Sekondari ya Kamugegi na hospitali ya wilaya Mwenyekiti wa LAAC, Mheshimiwa Staslaus Mabula(Mb) amesema kamati haijaridhishwa na utekelezaji wa miradi ya afya na elimu ya halmashauri hiyo. 


Amesema kuwa halmashauri hiyo haikufuata utaratibu na miongozo ya  ujenzi wa shule hiyo ikiwemo kutokufanyika kwa tathmini ya mchakato wa kupata mafundi wa ujenzi, kutokuandaliwa kwa mpango wa manunuzi na kutokufanyika kwa utafiti wa udongo.

Kutokana na hali hiyo, Kamati ya LAAC imeielekeza halmashauri hiyo kuhakikisha wanafuata miongozo na taratibu zilizowekwa katika kutekeleza miradi ya maendeleo kwa ufanisi ili iwe na tija 


Pia Kamati imependekeza kuwa halmashauri hiyo kuhakikisha inafanya marekebisho ya milango   na sakafu ya madarasa ili yaendane na hadhi ya madarasa yaliyojengwa 


"Kamati inaiagiza Halmashauri kuondoa milango ambayo haina ubora kwenye majengo yote ya shule na kuweka milango upya ili ifanane na uzuri wa madarasa," amesema Mhe.Mabula.


Kamati imeielekeza halmashauri  kupitia mapato ya ndani na fedha nyingine zitakazo toka  Serikali kuu kuhakikisha  wanarekebisha shule kwa ustadi kwa kuondoa maeneo yote yenye kasoro  na kuhakikisha shule inakamilika kwa ukamilifu wake na kuweza kutoa huduma. 


Shule ya Sekondari Kamugegi ni mojawapo ya shule za kata zilizojengwa kupitia  fedha za Mradi wa mpango wa kuboresha elimu ya Sekondari (Sequip), ambapo katika mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali ilipeleka Sh milioni 470 kwa ajili ya ujenzi wa shule hiyo.

Post a Comment

0 Comments