LAAC YAZITAKA HALMASHAURI KUWA WABUNIFU KWENYE MIRADI YA KIMKAKATI

 
Na Angela Msimbira, SIMIYU


Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali  Mitaa (LAAC) imetoa wito kwa halmashauri zote nchini kuwa wabunifu na kufikiria miradi mbadala ambayo itakuwa na uzalishaji bora na tija kwa halmashauri.


Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe.Staslaus Mabula wakati akikagua utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa jengo la wagonjwa wa dharura (EMD) pamoja na mradi mkakati wa ujenzi wa kiwanda cha chaki na vifungashio. 


Amesema kuwa kiwanda cha chaki ni mradi wa kimkakati wa pekee kwa kuwa halmashauri nyingi zinajenga stendi, masoko lakini halmashauri ya Wilaya ya Maswa imebuni mradi wenye tija kwa halmashauri ambao utasaidia kuongeza mapato yatakayonufaisha  jamii. 


Kamati imeiagiza Halmashauri ya Wilaya ya Maswa kuhakikisha kiwanda kinaanza kutumika ifikapo tarehe 15 Aprili,2024. 


Aidha, Kamati imeipongeza halmashauri hiyo kwa ujenzi mzuri wenye gharama halisi wa jengo la EMD katika Hospitali ya Wilaya ya Maswa.


Wamepongeza vifaa na vifaa tiba vilivyopo kwenye jengo ambavyo vinaonyesha nia na dhamira ya Serikali kuhakikisha suala la afya linakuwa ni kipaombele kwa watanzania kuanzia ngazi ya msingi ambapo lengo ni watanzania kupata huduma bora kuanzia ngazi ya zahanati, kituo cha afya na hospitali ya wilaya.


"Huwezi kuwa na jengo la dharura halafu halina vifaa vya msingi, hivyo nawapongeza halmashauri kwa kusimamia ujenzi na kuhakikisha linakamilika kwa wakati pamoja na kuanza kutoa huduma kwa jamii." 


Pia kamati imeshauri halmashauri hiyo kuhakikisha jengo linatuzwa na kutumika kwa lengo lililokusudiwa la kutoa huduma bora kwa wananchi.

Post a Comment

0 Comments