"MUHIMU WA SEKTA YA SHERIA KUTUMIA TEKNOLOJIA KWA UFANISI ILI KUFIKIA UPATIKANAJI WA HAKI NCHINI"RAIS DKT SAMIA

 
Na mwandishi wetu

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema ni Muhimu kwa sekta ya Sheria kutumia teknolojia kwa ufanisi ili kufikia upatikanaji wa haki nchini.


Hayo ameyasema huko Golden Tulip, uwanja wa ndege, wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Mawaziri wa Sheria wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Madola (Common Wealth).


Amesema  utumiaji wa Teknolojia katika sekta ya Sheria kutasaidia kuwepo uwazi kwenye masuala ya Sheria pamoja na kurahisisha upatikanaji wa haki sambamba na  kuimarisha ufanisi wa kazi  za Mahakama.


"Kupitia Teknolojia, Mahakama zinaweza kumudu uendeshaji wa kesi Kwa urahisi pamoja na kupunguza gharama  kubwa ya ufuatiliaji wa masuala ya haki." amesema Dkt Samia.


Dkt Samia ameishukuru Jumuiya ya Madola Kwa kuichagua Nchi ya Tanzania na hasa Zanzibar kwa kufanya Mkutano huo Mkubwa ambao unalenga uboreshaji wa upatikanaji wa haki.


Nae Waziri wa Katiba na Sheria wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Balozi. Dkt. Pindi Chana amesema Tanzania ni mfano Mkubwa wa demokrasia, Amani na Maendeleo chini ya uongozi wa Dkt Samia Suluhu Hassan.


Alieleza Rais Samia amekuwa ni kinara katika kusimamia  suala zima la Utawala wa Sheria Tanzania ili watanzania wapatiwe Hali zao katika Mahakama  kutokana na changamoto mbali mbali zinazowakabili. 


Kwa Upande wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais , Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora  Mhe. Haroun Ali Suleiman amesema Teknolojia ya Kidigitali ina msaada Mkubwa katika kutoa njia bunifu na rahisi Kwa watu katika ufikiaji wa haki zao.   


Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola Rt Patricia Scotland KC amesema  Mkutano huo ni wa kipekee ambao umehusisha mataifa 56 huru yanayozingatia masuala ya haki. 


Hata hivyo Rt Patricia amewashukuru  Watu wote wa Taifa la Tanzania licha ya kuwa katika huzuni kubwa ya Msiba wa mpendwa wao Rais wa Awamu ya Pili wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Marehemu Alhajj Ali Hassan Mwinyi  pia wameweza kuwapokea vizuri na wanajivunia kwa hilo. 


Mkutano wa siku tano wa  Mawaziri wa Sheria wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Madola anatarajiwa kufungwa  Tarehe 08 Machi 2024 na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi ukibeba  kauli mbiu  "Maendeleo ya Kidigitali yanavyoweza kutusaidia  upatikanaji wa haki".

Post a Comment

0 Comments