RAIS SAMIA NI KINARA UTEKELEZAJI WA MIRADI YA MAENDELEO - MAJALIWA.

 Na mwandishi wetu

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, amesema Rais Samia Suluhu Hassan ni kinara na kielelezo cha utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayoigusa jamii ya Watanzania.

 

Amesema kuwa maono na misingi  iliyojengwa na Rais, Dkt. Samia imewezesha Serikali ya awamu ya sita kutekeleza mipango mbalimbali ya maendeleo ikiwemo miradi ya kimkakati na kuimarisha utoaji wa huduma za jamii.

 

“Serikali imefanya mageuzi makubwa katika sekta ya usafiri na usafirishaji kwa kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya kuimarisha usafiri wa anga, usafirishaji kwa njia ya reli, barabara na usafiri katika bahari na maziwa makuu”.

 

Amesema hayo leo (Jumamosi, Machi 30, 2024) wakati wa Kongamano wa Maadhimisho ya miaka mitatu ya Rais Dkt. Samia lililofanyika Mkoani Mwanza.

 

Aidha,  amesema kuwa katika utekelezaji wa miradi ya usafiri katika maziwa makuu Serikalk imeendelea kutekeleza mradi wa ujenzi wa meli ya Mv. Mwanza Hapa Kazi Tu yenye uwezo wa kubeba abiria 1200, tani 400 za mizigo, magari madogo 20 na malori matatu na hadi sasa umefikia asilimia 94 ya ujenzi wake.

 

Amesema sambamba na ujenzi wa meli katika maeneo mbalimbali, Serikali pia imefanya maboresho katika bandari na kuongeza ufanisi wa utoaji huduma katika bandari hizo ikiwemo bandari kwenye Ziwa Victoria. 

 

Ameongeza kuwa  katika kuimarisha Sekta ya kilimo, Serikali imeendelea kuboresha usimamizi na utoaji wa huduma  kwa kuongeza Bajeti katika Wizara ya Kilimo.

 

“Serikali imeweka msisitizo katika usimamizi wa zao la Pamba ikiwemo kuongeza thamani ya zao hili nitoe wito kwa wakulima wa zao hili kuongeza uzalishaji ili mahitaji tuliyonayo yaendane na uhitaji uliopo”.

 

Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa Serikali inaendelea na ujenzi wa mradi wa Bandari ya Uvuvi pamoja na kutoa zana bora, pembejeo na vifaa muhimu vitakavyowawezesha kufanya shughuli zao kwa ufanisi lengo ni kuhakikisha sekta hiyo inachangia Pato la Taifa na uchumi wa mtu mmoja mmoja ikiwemo utekelezaji.

Post a Comment

0 Comments