SAFARI YA KUENDELEZA VYANZO VIPYA VYA UMEME YASHIKA KASI

 


Na mwandishi wetu

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko leo amezindua mradi mkubwa wa umeme Jua utakaozalisha megawati 150 katika Kijiji cha Ngunga wilayani Kishapu Mkoa wa Shinyanga ikiwa ni utekelezaji wa ahadi ya Serikali ya kuibua, kuendeleza na kutekeleza vyanzo mbalimbali vya umeme ili kuondokana na utegemezi wa Maji na Gesi Asilia kuzalisha umeme.


Dkt. Biteko amesema mradi huo utaanza kuzalisha megawati 50 ifikapo mwezi Januari mwaka 2025 na hii ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan la kuongeza vyanzo vya umeme kwani vilivyopo bado havitoshelezi mahitaji.


“Vyanzo vingine vya umeme tunavyoviendeleza ni pamoja na mradi wa Jotoardhi Songwe na Mbeya ambapo tarehe 1 Aprili mwaka huu uchorongaji unaanza katika eneo la Ngozi, mradi mwingine unaoenda kutekelezwa ni mradi wa megawati 100 wa upepo uliopo Makambako ambapo fidia imeanza kulipwa.” Amesema Dkt. Biteko 


Ameeleza kuwa kutekelezwa kwa mradi huo mkoani Shinyanga, kunafanya Mkoa huo kuwa kitovu cha umeme katika Ukanda wa Ziwa kwani mpaka sasa kuna vituo vikubwa vitatu vya umeme ambavyo ni Ibadakuli, Bulyanhulu na Buzwagi ambavyo vinasambaza umeme kwenye mikoa mbalimbali nchini.


Aidha amesema kuwa, kituo cha Ibadakuli kinaimarishwa ili kiwe kikubwa zaidi  na hivyo kuweza kusambaza umeme ndani na nje ya nchi kupitia makubaliano ya ushirikiano katika Sekta ya umeme kwa nchi za  Mashariki mwa Afrika  ambapo itajengwa laini kubwa ya msongo wa kV 400 kutoka Ibadakuli hadi Masaka Uganda ili kuunganisha Tanzania na Uganda kupitia Kagera.


Kuhusu usambazaji umeme vijijini Mkoa wa Shinyanga amesema kuwa, mkoa huo una Vijiji  509 ambapo vijiji 127 bado havijapata umeme.


Kufuatia hali hiyo, Dkt. Biteko amewataka wakandarasi  ambao wamechelewa kufikia lengo la usambazaji umeme kwenye mkoa huo kampuni ya Suma JKT na Tontan kuhakikisha kuwa wanamaliza kazi husika kwani uzembe kwenye miradi hiyo haukubaliki.


Vilevile, ameziagiza TANESCO na REA kuhakikisha kuwa wanawapelekea wananchi umeme kwa haraka na kama kuna changamoto ya umeme wananchi hao wapate taarifa mapema.
Post a Comment

0 Comments