BASHUNGWA AWAONDOA WATAALAM WOTE WANAOSIMAMIA UJENZI WA BARABARA YA KIBAONI - MLELE

 Na mwandishi wetu

Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa ameagiza kuondolewa kwa wataalam wote wanaosimamia ujenzi wa Barabara ya Kibaoni - Sitalike, sehemu ya kwanza ya Kibaoni - Mlele (km 50) kwa kiwango cha lami kutokana na ujenzi wa mradi huo kusuasua na utekelezaji wake kuwa nyuma kwa asilimia 23.71.

Ameagiza kuondolewa kwa Wataalam wote wa Mhandisi Mshauri wa Mradi Kampuni ya Crown Tech,  Msimamizi wa Mradi kutoka Makao makuu ya TANROADS, Eng. Ramadhan Myanzi pamoja na Msimamizi wa Mradi Mkoa wa Katavi, Eng. Albert Laizer.

Bashungwa ametoa agizo hilo Aprili 08, 2024 mkoani Katavi wakati akizungumza na wananchi wa Kata ya Kibaoni, Mkoani Katavi mara baada ya kukagua mradi huo ambao kwa sasa umefikia asilimia 14.7 na kutoridhishwa na kasi ya usimamizi na utekelezaji wa mradi huo.

“Mtendaji Mkuu wa TANROADS ninakuagiza watumishi wote ambao wapo chini ya Crown Tech wanaosimamia mradi pamoja na Msimamizi wa mradi kutoka TANROADS wote waondoke mara moja waje wapya, Nataka hii kazi ifanyike usiku na mchana barabara hii ikamilike kama ilivyopangwa”, amesema  Bashungwa.

Aidha, Bashungwa amebaini ubovu wa mitambo mingi ya Mkandarasi na amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi kupeleka timu ya wataalamu kufanya ukaguzi wa mitambo iliyopo eneo la mradi na kutambua mingapi inafanya kazi na mingapi haifanyi kazi pamoja na kuchukua hatua za kimkataba kwa Mkandarasi na Mhandisi Mshauri.

Bashungwa amemuagiza Msajili wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB) kuanza kumkagua Mkandarasi CRSG ambaye amekuwa akisumbua katika miradi mingi pamoja na kufika katika mradi huo kuangalia kwa mujibu wa sheria kama anafaa kuendelea kupata kazi na hatua za kisheria zichukuliwe.

Bashungwa amebainisha miradi ya barabara inayoendelea katika Mkoa wa Katavi ambayo inaunganisha na Mkoa wa Kigoma na kusema kuwa  tayari Serikali imekamilisha ujenzi wa barabara ya Mpanga - Vikonge (km 37) kwa kiwango cha lami.

Ametaja miradi mingine inayoendelea ikiwemo barabara Vikonge - Luhafwe (km 25) ambayo upo asilimia 57.4 na unagharimu Bilioni 35.6, barabara ya Luhafwe - Mishamo (km 37) upo asilimia 10 ya utekelezaji na unagharimu Bilioni 58.3 pamoja na barabara inayoelekea Bandari ya Kalema kutoka Kagwira zaidi ya kilometa 112 Mkandarasi ameshapatikana na mwaka huu barabara hiyo itaaza kujengwa kwa kiwango cha lami.

Akitoa taarifa ya mradi, Kaimu Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Eng. Doroth Mtenga ameeleza ujenzi wa barabara hiyo unagharamu kiasi cha Shilingi Bilioni 88.725 kutoka fedha za Mfuko Mkuu wa Serikali kwa asilimia 100 na umezalisha ajira 109 ambapo Waajiriwa 90 sawa na asilimia 82.57 ni Watanzania.

Mtenga ametaja sababu za mradi huo kuwa nyuma ya utekelezaji wake ukilinganisha na Mpango kazi pamoja na muda wa Mkataba uliokwisha pita ikiwemo Mkandarasi kutofwata mpango kazi uliothibitishwa pamoja na kuchelewesha kuleta wataalam wote kwenye mradi kama inavyotakiwa Kimkataba.


Post a Comment

0 Comments