LHRC YACHAMBUA SHERIA ZA UCHAGUZI BAADA YA KUSAINIWA NA RAIS

 Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) Dkt. Anna Henga (Wakili) akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.

NA MWANDISHI WETU

KITUO cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimefanya uchambuzi kuhusu Sheria za Uchaguzi baada ya kusainiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Aprili 4, 2024 jijini Dar es Salaam Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC Dkt. Anna Henga (Wakili) ameziainisha Sheria hizo kuwa ni Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya 2024.

Nyingine ni Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ya 2024 na Sheria ya Masuala ya Vyama vya Siasa na gharama za Uchaguzi, zilizopitishwa na Bunge baadaye kusainiwa na Rais.

"Tamko hili linatolewa kwa msingi wa kwamba, LHRC imehusika kikamilifu katika jitihada za uchechemuzi na maboresho ya mfumo wa Uchaguzi na vyama vya siasa, pia kama mdau aliyefanya uchambuzi na baadaye kuwasilisha maoni mbale ya Kamati ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria jijini Dodoma," amesema Dkt. Henga na kuongeza,

"Niwazi kwamba, kuletwa kwa miswada hiyo kulileta matumaini mapya katika Taifa la Tanzania, kufuatia hitaji la muda mrefu juu ya maboresho ya mfumo wa Uchaguzi na vyama vya Siasa. Hata hivyo wadau tulitegemea kuletwa kwa Muswada mwingine wa mabadiliko ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977 ili kuipa maana zaidi nia ya kufanya maboresho ya mifumo hiyo,".

Hivyo LHRC imeendelea kuirai Serikali kuleta Muswada wa mabadiliko ya Katiba, 2024 ili kufanikisha maboresho makubwa yanayotarajiwa kama ilivyopendekezwa na wadau pamoja na mapendekezo ya ripoti ya kikosi kazi cha Demokrasia ya vyama vingi iliyowasilishwa na Mwenyekiti wa kikosi hicho Prof. Rwekaza Mukandala Oktoba 21, 2022.

Kwamba pamoja na msisitizo huo, LHRC imebaini masuala chanya yaliyomo katika Sheria hizo Mpya, ametaja masuala hayo kuwa ni pamoja na Wakurugenzi wa Halmashauri za Manisapaa, Jiji na Wilaya kuondolewa kuwa wasimamizi wa Uchaguzi ingawa wamebaki kuwa waandikishaji wa Uchaguzi.

Mengine ni Sheria imeweka sifa ya mtu kuwa msimamizi wa Uchaguzi, Mosi, awe hajawahi kutiwa hatiani katika shauri la nidhamu au kosa lolote la jinai, pili, awe hajawahi kuadhibiwa kwa kifungo kinachozidi miezi sita na tatu, awe hajawahi kuwa Kiongozi wa Chama cha siasa.
Vile vile Sheria imefuta suala la wagombea kupita bila kupingwa katika ngazi zote (Rais, Ubunge na Madiwani) na Sharti la Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti na Wajumbe wa Tume kufanyiwa usaili na Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji kusimamiwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi.

Kadhalika kufutwa kwa sharti la kulipa ada yakupata upya kadi ya mpiga kura iliyoharibika au kupotea, pamoja na mashauru ya Uchaguzi kusikilizwa ndani ya miezi sita, na nafasi ya kiti cha Ubunge tofauti na pendekezo la miezi 12 kama ilivyokuwa kwenye Muswada.

"Hata hivyo mashauru ya Uchaguzi kwa ngazi ya udiwani yatasikilizwa kwa miezi 12 ambayo bado tunaona ni muda mrefu," amesema Dkt. Henga.

Hata hivyo ametoa wito kwa Serikali kuwasilisha Muswada wa Sheria utakaotoa fursa ya kufanya mabadiliko ya Katiba ili kuruhusu baadhi ya Masuala ambayo kwa uasili wake hayawezi kufanyiwa marekebisho bila kugusa Katiba.

Post a Comment

0 Comments