MAKAMU WA RAIS MHE. Dkt. PHILIP MPANGO AFUNGUA SKULI YA SEKONDARI YA MAZIWANG’OMBE - PEMBA

 


Na mwandishi wetu


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango ametoa wito kwa wazazi na walezi kusimamia kikamilifu elimu ya watoto kwa kudhibiti utoro katika skuli pamoja na kuhakikisha watoto wa kiume na wa kike wanaojiunga na skuli za msingi na sekondari wanamaliza masomo.

 

Makamu wa Rais ametoa wito huo wakati wa Ufunguzi wa Skuli ya Sekondari Maziwang’ombe iliyopo Wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba ikiwa ni Shamrashamra za Maadhimisho ya Miaka 60 ya Muungano. Amesema ni vema kuwaandikisha watoto wote wenye umri wa kwenda skuli, kuwafuatilia maendeleo yao pamoja na kuwahimiza kusoma badala ya kushiriki katika shughuli za uvuvi na nyinginezo. Amewasihi kutumia vema miundombinu bora ya elimu iliyoandaliwa na serikali ili kuhakikisha watoto wanapata elimu bora.

 

Aidha Makamu wa Rais amesisitiza umuhimu wa jamii kushirikiana katika malezi ya watoto kwa kufuata mila na desturi sahihi, maadili yaliyo mema na kushika mafundisho ya dini ambayo yatawaepusha na maovu mengi katika jamii inayowazunguka. Ametoa wito wa kuhakikisha hatua za kisheria zinachukuliwa kwa watakaobainika kufanya unyanyasaji wa kijinsia na kingono, kuoa au kusababisha mimba za utotoni ili kuzuia tabia ya watoto kukatishwa masomo.

 

Makamu wa Rais ameongeza kwamba Serikali zote mbili zimedhamiria kuleta usawa wa kijinsia kwa kuondosha mila na taratibu kandamizi. Ametaja tatizo la ndoa za mapema Kaskazini Pemba linaathiri ustawi wa watoto wa kike na hivyo kuwanyima fursa mbalimbali katika maisha.

 

Vilevile Makamu wa Rais amehimiza umuhimu wa kushirikiana katika kulinda na kutunza mazingira. Amesema uchafuzi na uharibifu wa mazingira hapa nchini kutokana na shughuli mbalimbali bado ni tatizo kubwa ambapo jitihada kubwa za Serikali za maendeleo zinaathiriwa na changamoto hiyo.  

 

Ametoa rai kwa Wakuu wa Skuli zote kuhakikisha kila mwanafunzi anaotesha walau mti mmoja (matunda na kivuli) na kuutunza kwa kipindi chote atakachokuwepo skuli.  Aidha amewasihi wananchi kuotesha miti na kuitunza katika makaazi yao na maeneo mengine.

 

Makamu wa Rais amesema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, zimejizatiti kuendelea kuulinda na kuuimarisha Muungano kwa lengo la kudumisha amani, utulivu na kuwaletea wananchi wote maendeleo. Amesema katika kipindi cha miaka 60 ya Muungano mafanikio makubwa yamepatikana katika sekta ya elimu ikiwemo Elimu kuwa ni haki ya msingi ya kila Mtanzania, Ongezeko la miundombinu ya elimu, Ongezeko la vyuo na taasisi za Elimu ya Juu pamoja na Ongezeko la Idadi ya wanafunzi kutoka Zanzibar wanaopata mikopo ya Elimu ya Juu

 

Amesema jitihada hizo za Serikali katika kuimarisha miundombinu ya elimu ni endelevu na zinajumuisha upatikanaji wa vifaa mbalimbali vikiwemo vifaa vya kufundishia na kujifunzia, samani na upatikanaji wa walimu wenye sifa.

 

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali – Zanzibar Ali Abdulgalam Hussein amesema ufunguzi wa skuli hiyo ni matunda ya Muungano unaotimiza miaka 60. Amesema Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali itaendelea kutekeleza ilani ya uchaguzi kikamilifu ili kuhakikisha malengo yaliowekwa yanafikiwa.

 

Ujenzi wa Skuli hiyo ya ghorofa tatu umegharimu shilingi bilioni 6.2. Shule hiyo ni ya kwanza kwa upande wa sekondari katika kijiji cha Maziwang’ombe ambapo ina uwezo wa kuchukua wanafunzi 1850 kwa pamoja kwa wastani wa wanafunzi 45 kila darasa. 

Imetolewa na

Ofisi ya Makamu wa Rais

21 Aprili 2024

Pemba – Zanzibar.

Post a Comment

0 Comments