MRADI WA AWAMU YA PILI YA KUKINGA NA KUDHIBITI MARADHI YASIYO AMBUKIZA YAZINDULIWA ZANZIBAR

 


Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa Maradhi Yasiyoambukiza (ZNCDs)  Dkt . Said Gharib Bilali  amesema maradhi yasiyoambukiza yanahitaji kupewa kipaumbele kwa kuzingatia utoaji wa elimu na huduma sahihi za afya ili kuweza kuzuwia vifo vya mapema vinavyotokana na maradhi hayo.


Hayo yameelezwa wakati wa uzinduzi wa mradi wa awamu ya pili wa kukinga na kudhibiti maradhi yasiyoambukiza kuwa  kipaumbele cha Afrika Mashariki katika Jumuiya ya Umoja wa Watu Wanaishi na Maradhi Yasioambukiza Zanzibar huko Mpendae Wilaya ya Mjini.


Amesema ni vyema jamii kupatiwa elimu ya maradhi hayo ili kupata uwelewa wa kuweza kupambana nayo kutokana na vichocheo na athari zake.


Aidha ameeleza hatua ya  kupatiwa taaluma ya maradhi hayo na huduma bora za kiafya kutaisaidia jamii kujikinga na kujiwekea utaratibu wa  kuchunguza afya zao jambo ambalo litasaidia kupunguza  ongezeko la wagonjwa hao na kupambana na maradhi hayo.


Amefahamisha kuwa mashirikiano ya pamoja kwa wadau mbali mbali  pamoja na Serikali kutaongeza juhudi ya kupambana na changamoto ya maradhi yasioambukiza.


Nae Meneja wa Jumuiya ya Umoja wa Watu Wanaishi na Maradhi Yasioambukiza Zanzibar (ZNCDs) Haji Khamis Fundi amesema lengo la mradi huo ni kuihamasisha jamii kufuata maelekezo ya wataalamu ili kupunguza vifo vya mapema vinavyotokana na maradhi hayo.


“Jamii ikipewa uelewa wa kutumia mfumo bora wa ulaji kufanya mazoezi kuacha kutumia vilevi sigara na tumbaku, kupima afya kutasaidia kupunguza ongezeko la vifo ” amefahamisha Meneja huyo.


Kwa upande wa wanachama wa Jumuiya hiyo wakielezea changamoto mbali mbali wanazokumbana nazo ikiwemo kukosa huduma za NCD katika vituo vyao vya karibu pamoja na uhaba wa watoaji huduma za maradhi hayo .


Jumuiya ya maradhi yasioambukiza ni mkusanyiko wa Jumuiya za nchi mbali mbali za Afrika Mashariki ikiwemo Burundi,  Kenye,  Ruwanda, Tanzania, Uganda na Zanzibar zenye lengo la kupunguza vifo vya maradhi ya NCDs katika nchi zao.
Post a Comment

0 Comments