RAIS DK.MWINYI AZINDUA TAASISI YA WASANIFU NA WAHANDISI ZANZIBAR

 


Na mwandishi wetu

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi amesema utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo unazingatia dhana ya ushirikishwaji wa Wahandisi wa kitanzania kupitia miradi endelevu ya kimkakati ya uwekezaji nchini.


Rais Dk.Mwinyi amesema hayo alipozindua Taasisi ya Wasanifu , Wahandisi na Wakadiriaji Zanzibar na Mkutano mkuu wa mwaka huu katika ukumbi wa Hoteli ya Verde, Mkoa wa Mjini Magharibi tarehe 20 Aprili 2024.


Aidha Rais Dk.Mwinyi amesema Serikali zote mbili ya Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zinafanya jitihada  ikiwemo kuweka mazingira wezeshi kujiajiri, kuhamasisha utambuzi wa fursa mbalimbali, kurejesha stadi  za ujuzi, elimu ya uanagenzi vyuoni pamoja na kutenga bajeti kwa ajili utafiti na ubunifu mbalimbali. 


 Rais Dk.Mwinyi ameeleza kuwa Serikali  kwa upande wake kupitia Uchumi wa Buluu imeendeleza sera ya kuajiri wasanifu, wahandisi na wakadiriaji wazalendo.


Halikadhalika Rais Dk.Mwinyi amesema Serikali inathamini mchango wa fani mbalimbali katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo ikiwemo miradi ya ujenzi.


Kwa upande mwingine Rais Dk.Mwinyi amewapongeza wakandarasi na washauri wazawa kwa kufanya kazi za uhandisi kwa ufanisi katika miradi mbalimbali waliyotekeleza.

Post a Comment

0 Comments