TIC IMEKUWA INJINI KUTEKELEZA MAONO YA RAIS DKT. SAMIA - MAJALIWA.

 


Na mwandishi wetu

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameupongeza uongozi na wafanyakazi wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kwa kuwa injini ya kutekeleza maono ya Rais wa Jamhuri ya Muuumgano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kujenga Tanzania yenye mvuto kwa wawekezaji wote.


“Hatua ambayo nchi yetu imefikia kwa sasa, inaondoa shaka kwa wawekezaji na imeendelea kuthibitisha kuwa nchi yetu ni salama kwa wote waliotayari kuwekeza mitaji yao. Endeleeni kuwa wabunifu, kuimarisha utoaji huduma na kukidhi mahitaji ya ushindani katika masoko ya uwekezaji.”


Mheshimiwa Majaliwa amesema Serikali ya awamu ya sita imeleta mageuzi makubwa kwa kufanya maboresho mbalimbali katika mifumo, sera na sheria ili kuboresha mazingira ya biashara na kuvutiauwekezaji hapa nchini. 


“Kipindi cha miaka mitatu ya mageuzi kimedhihirisha matokeo ya dhamira njema ya Mheshimwa Rais katika kukuza diplomasia ya kiuchumi na kujenga mazingira bora na rafiki ya uwekezaji hapa nchini.”


Ameyasema hayo leo (Jumapili Aprili 28, 2024) wakati alipokuwa akifungua Semina Maalum ya uwekezaji kwenye kilimo iliyoandaliwa na benki ya CRDB katika Ukumbi wa The Super Dome Masaki, Jijini Dar es Salaam.


Amesema Serikali imeimarisha utoaji huduma kwa wawekezaji kwa kuimarisha Kituo cha Utoaji wa Huduma za Mahali Pamoja kilichoko TIC ambapo kwa kwa sasa taasisi 14 za Serikali zinatoa huduma katika Kituo cha mahali pamoja.


Amezitaja taasisi hizo kuwa ni Wizara ya Kazi, Wizara ya Ardhi, Uhamiaji, NIDA, NEMC, TRA, Wizara ya Kilimo, Wizara ya Madini, BRELA, TBS, TMDA, OSHA, TANESCO na TIC yenyewe.
Post a Comment

0 Comments