WAUZA BIDHAA NJE YA NCHI WAHIMIZWA KUZINGATIA SHERIA

 


Wauza Bidhaa nje ya nchi wahimizwa kuzingatia sheria


Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania amewahimiza wauzaji wa bidhaa na huduma nje ya mipaka ya Tanzania kuzingatia Kanuni za Fedha za Kigeni katika kufanya biashara zao ili kuepuka uuzaji na utumiaji holela wa fedha za kigeni.


Ameyasema hayo alipokutana na wafanyabiashara hao leo tarehe 5 Aprili, 2024 katika Ofisi ya Makao Makuu Ndogo ya Benki Kuu ya Dar es Salaam.


“kanuni za fedha za kigeni za mwaka 2023 zinamtaka muuzaji wa bidhaa na huduma nje ya nchi kuhakikisha fedha zitokanazo na mauzo hayo zinawekwa kwenye akaunti zao za benki hapa nchini ndani ya siku 90. Hata hivyo, tumegundua kwamba baadhi wa wauzaji wa bidhaa na huduma nje ya nchi (exporters) hawatimizi takwa hili la kisheria” amesema Gavana.


Ameongeza kuwa Benki Kuu imebaini uuzaji holela wa fedha za kigeni miongoni mwa wafanyabiashara hao na amezitaka benki kusitisha huduma kwa wateja wasiotimiza matakwa haya ya kisheria. 


Aidha, Gavana Tutuba amesema kurejeshwa kwa Mfuko wa Udhamini wa Mikopo kwa ajili ya Mauzo Nje ya Nchi (ECGS)na Mfuko wa Udhamini wa Mikopo kwa Wajasiriamali Wadogo na wa Kati (SMEs-CGS) unalenga kuongeza mauzo ya bidhaa nje ya nchi na kutengeneza mazingira mazuri na wezeshi kwa washiriki wa sekta hiyo ambao aliwataja kuwa wadau muhimu na katika kutunisha akiba ya fedha za kigeni.


Naye Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Biashara (TCNBC),Dkt. Godwill Wanga, ameipongeza Benki Kuu kwa hatua mbalimbali ilizochukua katika kukabiliana na upungufu wa fedha za kigeni na uchumi kiujumla kupitia kuanza kutumia mfumo wa sera ya fedha unaotumia riba ya Benki Kuu.


Aliongeza kuwa hatua mbalimbali zinazochukuliwa na serikali na Benki Kuu zimefanya upungufu wa fedha za kigeni uliopo nchini kuwa himilivu ukilinganisha na hali iliyopo katika nchi nyingine ulimwenguni.


Kwa upande wa washiriki wa mkutano huo, wameipongeza BoT kwa mchango wake katika kustawisha sekta ya fedha nchini na wameahidi kushirikiana na BoT katika kutoa elimu ya uuzaji holela wa fedha za kigeni.

Post a Comment

0 Comments