WAZIRI JAFO AFANYA MAZUNGUMZO NA WAZIRI WA USHIRIKIANO WA MAENDELEO NA SERA ZA MABADILIKO YA TABIANCHI WA DERNMARK

 


Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Ushirikiano wa Maendeleo na Sera za Mabadiliko ya Tabianchi wa Denmark Mhe. Dan Jørgensen.


Katika mazungumzo yao yaliyofanyika leo Aprili 05, 2024 jijini Dodoma, viongozi hao wamejadili ushirikiano wa nchi hizo mbili katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na mazingira kwa ujumla.


Dkt. Jafo amemueleza Waziri Jørgensen dhamira ya Serikali ya Tanzania katika kuchagiza upatikanaji wa nishati safi ya kupikia ili kukabiliana na changamoto ya ukataji wa miti ikiwa ni katika kuhakikisha hifadhi ya mazingira inakuwa endelevu.


Amemuahidi kuendeleza ushirikiano uliopo kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Denmark huku akisema utaleta mafanikio katika utekelezaji wa miradi ya mazingira hapa nchini.


Pia, amemuelezea kuhusu namna Serikali ya Tanzania kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais inavyokabiliana na athari za uharibifu wa mazingira hususan mabadiliko ya tabianchi kupitia mikakati mbalimbali.


Aidha, Waziri Dkt. Jafo ameongeza kuwa kupitia ziara ya kiongozi huyo, wadau mbalimbali wa mazingira wa Tanzania watajifunza masuala mbalimbali hususan ya ubunifu wa teknolojia ya nishati safi.


Amewaomba Watanzania kutumia wigo wa fursa zinazotokea kutokana na diplomasia ya uchumi iliyojengwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia ziara zake katika mataifa mbalimbali.


Kwa upande wake Waziri Jørgensen amesema ni wakati sasa wa kudumisha uhusiano baina ya nchi hizo mbli ili kupambana na mabadiliko ya tabianchi yanayoikabili dunia.


Amesema kuwa mabadiliko ya tabianchi yana athari kubwa katika nchi mbalimbali duniani ikwemo Tanzania na kuathiri shughuli za kiuchumi husausan kilimo hivyo ni muhimu kuunganisha nguvu kukabiliana nayo.


Kikao hicho kimehudhuriwa na Mkurugenzi wa Mazingira Bi. Kemilembe Mutasa, Mkurugenzi wa Sera na Mipango Bw. Ignas Chuwa, Mkurugenzi Msaidizi wa Mazingira Dkt. Paul Deogratius Paul (kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais).Post a Comment

0 Comments