WAZIRI MKUU AFUNGA MAONESHO YA WIKI YA NISHATI 2024

 


Na mwandishi wetu

📌 *Atoa maagizo mahsusi kwa Wizara ya Nishati*


📌 *Ataka maonesho yafanyike hadi ngazi za Mikoa, Wilaya*


📌 *Apongeza Wizara kwa utulivu wa hali ya umeme nchini*


📌 *Zaidi ya asilimia 70 ya Wabunge watembelea Maonesho*


Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa amefunga Maonesho ya Wiki ya Nishati katika Viwanja vya Bunge jijini Dodoma kutoa maagizo kwa Wizara ya Nishati na Taasisi zake kuendelea kuboresha maonesho hayo na utoaji wa huduma kwa wananchi.


Mhe. Majaliwa ameitaka Wizara ya Nishati kuweka mkakati wa kuhakikisha maonesho hayo yanakuwa endelevu ili wabunge wapate fursa za kuwasilisha hoja zao moja kwa moja kwa wataalam na kupewa majawabu ya hoja na changamoto zinazowakabili wao na wananchi wanaowakilishwa.


Aidha, ameagiza Maonesho ya Nishati yafanyike kuanzia ngazi ya wilaya, mikoa na halmashauri ili yale yanayofanyika Makao Makuu yabaki kuwa ya Kitaifa. 


Amefafanua kuwa kwa kufanya hivyo huduma zitakuwa zimesogezwa zaidi kwa kwa wananchi na  pia Mameneja wa TANESCO wa Kanda, Mikoa na Wilaya watoe ufafanuzi wa hoja na changamoto zinazowakabili wananchi husika.
Vilevile ameitaka Wizara kuweka mkakati wa kuwawezesha wananchi wote kupata ufafanuzi na fursa zinazotokana na miradi inayotekelezwa katika Sekta ya Nishati.


Pia ameagiza maonesho hayo yafanyike maeneo yanayofikika kwa urahisi kwa wananchi wengi kama vile katikati ya miji ili wananchi wengi washiriki na kupata ufafanuzi wa masuala mbalimbali.


Vilevile Waziri Mkuu ameitaka  Wizara isimamie na kuondoa mlundikano wa maombi ya kuunganisha umeme kwa wananchi na TANESCO ihakikishe inaimarisha mfumo wa kupokea maombi na kutekeleza maombi hayo kwa haraka.


Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ametoa agizo kuwa Taasisi zote zinazolisha watu wengi kuanzia  50 hadi 100 waanze kubadilisha teknolojia ya kupikia na kutumia Nishati Safi ya Kupikia na ifikapo mwisho wa mwaka 2024 Serikali inataka kuona asilimia 99 ya Taasisi za aina hiyo zinatumia Nishati Safi ya Kupikia.

Vilevile amempongeza Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati  kwa utendaji kazi wake ambao umechochea hali ya upatikanaji umeme nchini kuongezeka na kutosheleza mahitaji na  pia kuwezesha upatikanaji wa umeme wa ziada.


Kwa upande wake, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Doto Biteko amelipongeza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa kuendelea kuboresha utoaji huduma ya umeme nchini.


Amesema,  “ tunafanyakazi  kubwa kubadilisha taswira ya Wizara ya Nishati na Taasisi zake na niwashukuru sana watendaji wa Wizara hii na Taasisi zake kwa kufanyakazi kwa juhudi na niwaombe waongeze kasi.” Amesema Dkt. Biteko.


Amewapongeza wakandarasi wa umeme kwa kuendelea na utekelezaji wa miradi ya nishati katika maeneo mbalimbali nchini, sambamba na kuvipongeza vyombo vya habari nchini kwa kuendelea kutangaza habari zinazohusu masuala ya nishati kwa lengo la kujibu hoja na maswali mbalimbali ya wananchi.


Kwa upande wake, Spika wa Bunge Mhe. Dkt. Tulia Ackson, amesema kuwa sekta ya nishati ni moja kati ya sekta mtambuka nchini inayochagiza maendeleo ya Sekta nyingine na kwamba ili maendeleo yapatikane sekta ya nishati ina mchango mkubwa.


Ameeleza mchango sekta ya umeme hauepukiki katika ngazi zote kuanzia vitongoji hadi Taifa huku sekra ya uzalishaji ikiwemo viwanda na migodi na maeneo mbalimbali huku akisisitiza kuwa umeme usitumike kwa ajili ya mahitaji ya awali pekee kama kuwasha taa na kuchaji simu.


Akizungumzia mradi wa kuzalisha umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) amesema, “Bwawa la Julius  Nyerere licha ya kuzalisha umeme litasaidia masuala mbalimbali ikiwemo upatikanaji wa maji hasa mikoa ya karibu na bwawa hivyo  badala ya maji kupita tu kwenye mkondo wa maji basi yahifadhiwe kwa ajili ya kusambaza kwa wananchi”. Amesema Mhe. Tulia.


Aidha, Mhe. Spika ameishauri Serikali kuanzisha gridi ya maji kama ilivyo gridi ya umeme ambayo ipo katika maeneo mengi nchini ili kusaidia usambazaji wa maji katika maeneo kame kwa kutumia gridi ya maji.


Naye, Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Mhe. David Mathayo ameipongeza Wizara ya Nishati kwa kuandaa maonesho ya Wiki ya Nishati ambayo yametoa fursa kwa Waheshimiwa Wabunge na wananchi kupata uelewa kuhusu utekelezaji wa kazi zinazofanywa na Wizara ya Nishati pamoja na Taasisi zake na kushauri maonesho hayo kuwa endelevu.

Amesema Kamati yake itaendelea kushauriana na Wizara katika masuala mbalimbali yanayohusu nishati ikiwemo upelekeji wa huduma kwa wananchi wanaozunguka miradi mbalimbali hasa ya Gesi Asilia ili maisha yao yaendane na thamani ya miradi hiyo.


Awali, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba alisema kuwa Wiki ya Nishati kwa mwaka 2024 imekuwa na mafanikio makubwa kutokana na kuhudumia idadi kubwa ya Waheshimiwa Wabunge na wageni mbalimbali.


“Wabunge  267 wametembelea mabanda ya maonesho na kujionea kazi zinazofanywa na Wizara na Taasisi zake,  kuuliza maswali na kutoa maoni na wananchi 213 walitembelea maonesho haya” amesema Mhandisi Mramba.

Post a Comment

0 Comments