BRELA KUNOGESHA SIKU YA MILIKI BUNIFU,DKT KIJAJI NA MWANA FA WAGENI RASMI.

 


Na mwandishi wetu

WAKALA wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) inaungana na Shirika la Miliki Ubunifu Duniani (WIPO) na Nchi nyingine kuadhimisha siku ya Miliki Ubunifu Duniani ambayo huadhimishwa Aprili, 26 kila mwaka ambapo kwa Tanzania yatafanyika kesho Mei 9, 2024 jijini Dar es Salaam.


Akizungumza na waandishi wa habari leo Mei 8, 2024 jijini Dar es Salaam Mkurugenzi wa Miliki Bunifu wa BRELA Loy Mhando amesema lengo la maadhimisho hayo ni kukuza Vumbuzi na Bunifu mbalimbali kwa manufaa ya baadaye na kutambua mchango wa ubunifu katika kufikia maendeleo endelevu.


Amesema maadhimisho hayo yanatarajiwa kuwa na ushiriki wa Dkt. Ashatu Kijaji, Waziri wa Viwanda na Biashara ambaye ndiye mratibu wa shughuli hiyo.


"Vile vile kutakuwa na ushiriki wa Mhe. Hamis Mwinjuma (Mb), Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Kauli mbiu ya maadhimisho ya siku ya Miliki Bunifu Duniani kwa mwaka 2024 ni "Miliki Ubunifu na Malengo ya Maendeleo Endelevu: Kujenga Mustakabali wa pamoja kwa kutumia Ubunifu (Intellectual Property and the SDGs: Building our Common further with Innovation and Creativity)," amesema Mhando.


Mhando ameeleza kuwa Shirika la Miliki Ubunifu Duniani (WIPO), ilianzishwa kwa lengo la kukuza na kulinda nyezo za Miliki Ubunifu ikiwemo Vumbuzi kwa kutoa Hataza, alama zinazowekwa kwenye bidhaa na huduma, hakimiliki na hakishiriki.


Kwamba Tanzania ni miongoni mwa Nchi wanachama wa WIPO, hivyo imekuwa ikiunga mkono na kushiriki katika jitihada zinazofanywa na Shirika hilo kwa kuhakikisha kuwa inakuza uelewa wa masuala ya Miliki Ubunifu pamoja na kuzilinda kisheria ili kwenda sambamba na mabadiliko ya Sayansi na Teknolojia na kukuza uchumi.


Amesema katika maadhimisho ya mwaka huu, amewaalika wadau mbalimbali ikiwa ni pamoja na Taasisi zinazosimamia masuala ya Miliki Ubunifu Tanzania Bara na Zanzibar, Taasisi za umma pamoja na sekta binafsi ili kujadili kwa pamoja fursa, mafanikio, na changamoto zilizopo katika nyanja ya Miliki Ubunifu.


Vile vile, baadhi ya wabunifu kutoka sekta mbalimbali watashiriki na kazi zao za Ubunifu zitaoneshwa.


Mhando amesema kuelekea maadhimisho hayo, maafisa wa BRELA na COSOTA wametoa elimu kuhusu Miliki Ubunifu katika baadhi ya Vyuo vya Elimu ya Juu, Vyuo vya Ufundi na Teknolojia, Waandishi wa Habari, Wazalishaji na Wajasiriamali.


Kwamba pamoja na kutoa elimu kupita vyombo vya Habari ikiwa ni njia mojawapo ya kuhamasisha wabunifu kuhakikisha wanaendeleza na kulinda Bunifu zao ili ziwapatie manufaa wao pamoja na Taifa kwa ujumla.


Amesema matukio katika maadhimisho haya, ni pamoja na mijadala kuhusu Miliki Ubunifu ambayo itahusisha Sekta za Umma na Binafsi ambao kwa pamoja watajadili kuhusu fursa, mafanikio, na changamoto wanazokutana nazo katika nyanja ya Miliki Ubunifu.


Kadhalika ameeleza kuwa hati za makubaliano ya ushirikiano katika eneo la Miliki Ubunifu baina ya BRELA, COSOTA na Taasisi nyingine zitasainiwa ikiwa ni njia ya kurasimisha ushirikiano ulipo baina ya Taasisi hizo katika kuhakikisha Miliki Ubunifu inaleta manufaa katika Maendeleo ya kiuchumi

Post a Comment

0 Comments