DKT. NDUGULILE AMETEULIWA KUGOMBANIA MKURUGENZI MKUU WA W.H.O KANDA YA AFRIKA

 Na mwandishi wetu

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan amemchagua na kumpendekeza Dkt. Faustine Ndugulile kugombea nafasi ya Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani Kanda ya Afrika ambapo ni kwa mara ya kwanza Tanzania inatoa mgombea wa nafasi hiyo.Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amesema hayo leo Mei 8, 2024 wakati wa uzinduzi wa kampeni za kugombea nafasi hiyo aliyopendekezwa Dkt. Faustine Ndugulile mwenye uzoefu na ujuzi mkubwa katika masuala ya Afya duniani ambae pia ni Daktari wa Taaluma hiyo.

“Tanzania ni miongoni mwa nchi ambazo zinafanya vizuri sana duniani katika mapambano dhidi ya magonjwa ya kuambukiza, magonjwa yasiyoambukiza pamoja na kuimarisha huduma za afya ya uzazi mama na mtoto, Tanzania tumefanikiwa kupunguza vifo vya wanawake wajawazito kwa zaidi ya asilimia 80″. Amesema Waziri Ummy.

Amesema, Tanzania ina mfumo mzuri sana wa kuimarisha huduma za Afya ngazi ya msingi kuanzia Zahanati, Vituo vya Afya pamoja na Hospitali za Halmashauri, hivyo itakwenda kubadilishana uzoefu huo na nchi nyingine za Afrika.

“Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani Kanda ya Afrika ambae anamaliza muda wake wa miaka 10 anatokea nchini Botswana ukanda wa SADC, kwa Tanzania ni Mara ya kwanza tunagombea nafasi hiyo na tunaamini kabisa tutashinda nafasi hiyo kutokana na aina ya mgombea ambae tumemuweka.” Amesema Waziri Ummy.

Kwa upande wake Dkt. Faustine Ndugulile ambae ndio mgombea wa nafasi hiyo amemshukuru Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kupendekeza jina lake na kuridhia kugombea katika nafasi hiyo.

“Nafasi hii inasimamia nchi 47 katika Bara la Afrika, Tanzania tunafanya vizuri sana katika Sekta ya Afya na tuna mafanikio makubwa ya kuigwa, tunataka na sisi tuende tukayaeneze yale mazuri yetu kwa wengine ili kuweza kusimama pamoja”. Amesema Dkt. Ndugulile.

Dkt. Ndugulile amebainisha vipaumbele vya nchi ambavyo ni pamoja na kuendelea kuboresha huduma za Afya katika kupunguza vifo vya mama na mtoto ambalo ni eneo Tanzania tumefanya vizuri, nchi nyingi za Afrika bado wana changamoto hiyo.

Pia, amesema Tanzania inataka ikasimamie kujenga mifumo imara ambayo itaweza kuhimili athari za magonjwa ya milipuko pamoja na majanga mengine ambapo kwa Bara la Afrika limeathirika sana na magonjwa hayo. 

Post a Comment

0 Comments