SERIKALI ITAENDELEA KUTOA USHIRIKIANO KWA TAASISI ZA DINI- DK.MWINYI

 Na mwandishi wetu


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali itaendelea kutoa ushirikiano kwa Taasisi za Dini ili ziweze kufanya shughuli zao kwa uhuru na kushirikiana kutoa huduma mbalimbali kwa jamii na kutatua changamoto zao.


Rais Dk.Mwinyi amesema hayo wakati wa Ibada Kuu ya Upatanisho na Msamaha kutokana na madhila ya biashara ya utumwa iliyofanyika kwenye Kanisa la Anglikana Tanzania Dayosisi ya Zanzibar Kanisa Kuu la Kristo , Mkunazini Mkoa wa Mjini Magharibi na kuongozwa na Askofu Mkuu wa Canterbury, Mhashamu Justin Welby tarehe 12 Mei, 2024.


Aidha Rais Dk.Mwinyi ameridhia ombi la Kanisa la Anglikana Tanzania la kutaka kuifanya Juni 6 ya kila mwaka kuwa siku maalum ya kumbukumbu kuondolewa biashara ya utumwa. 


 Rais Dk.Mwinyi amewashukuru viongozi wa Madhehebu ya Dini kwa kuendelea kuhubiri amani, umoja na mshikamano na kuwahimiza waumini wote kudumisha tunu hizo muhimu kwa taifa letu. 


Kwa upande mwingine Rais Dk.Mwinyi ameeleza kuwa Serikali imesamehe kodi ya makusanyo ya watalii eneo la kihistoria la Kanisa Kuu la Kristo Mkunazini, pia ameiagiza Wizara ya fedha, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na Wilaya kushughulikia kwa utaratibu mzuri wa makusanyo katika eneo hilo  .Post a Comment

0 Comments