WAVAMIA MSITU WA HIFADHI NA KUFANYA MAUAJI KILOSA.

 📍Kilosa, Morogoro 


🗓️ 10 Mei 2024

*Dc  Shaka alani vikali, mmoja atiwa mbaroni mwingine aendelea kusakwa*


Na Mwandishi Wetu.


MKUU wa Wilaya ya KIlosa mikoani Morogoro, Shaka Hamdu Shaka amesema kuwa vyombo vya ulinzi na usalama wilayani humo vinamshikilia Dotto Lusuka (21) huku vikiendelea kumsaka Suma Lusaka kwa tuhuma za kuhusika na mauaji ya Lazaro Ndutu, katika Kitongoji cha Kikuyu, Kijiji cha Kigunga, Kata ya Zombo, Tarafa ya Ulaya.


Akithibitisha kwa vyombo vya habari kuhusu mauaji hayo, Shaka alisema tukio hilo lilitokea jana saa 2 asubuhi  ndani ya hifadhi ya msitu wa kijiji hicho, chanzo ikisadikiwa ni ugomvi uliisababishwa na kuwania eneo msituni humo.


Kwa mujibu wa Shaka ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama ya Wilaya hiyo, baada ya tukio hilo ndugu walimkimbiza hospitali Ndugu, lakini baadaye alifariki Dunia usiku wa kuamkia leo.


Shaka alisema kuwa Machi mwaka huu, alipokea taarifa za wananchi kuvamia msitu huo na serikali ikachukua hatua za kupiga marufu uvamizi huo na kufanya doria kudhibiti vitendo hivyo.


"Ni kweli vyombo vya Ulinzi na Usalama vinamshikilia kijana Dotto John Lusuka (Msukuma) miaka 21 kwa tuhuma za kuhusika na mauji hayo ambapo  kijana mwingine Suma John Lusaka  mdogo wa mtuhumiwa aliyekamatwa, naye anatafutwa na jeshi la polisi baada kutoroka baada ya tukio.


"Tulipiga marufu na kuimarisha doria katika hifadhi za misituni baada kupata taarifa za uvamizi na kulielekeza Jeshi la Polisi, TFS na halmashauri kusimamia matumizi na kulinda hifadhi za misitu  pamoja na juhudi kadhaa kuchukuliwa.


"Licha ya hatua hizo wananchi wamekuwa wakivamia kwa siri na wakati mwingine kutaka kujichukulia sheria mkononi, kukata miti, kuingiza mifugo,  kuchoma mkaa na kufanya uharibifu wa mazingira," alisema Shaka.


Alibainisha kuwa mipango ya serikali ni kuhakikisha kuwa hifadhi za  misitu na rasimali zote muhimu  wilayani humo zinaendelea kuwekewa mikakati madhubuti ili kunusuru athari zaidi za kimazingira na maafa makubwa kuweza  kutokea


"Serikali inalaani vikali mauaji  haya ambayo kimsingi ni kinyume na utu na ubinadamu, kitendo cha kumkata kata binadamu mwenzio kama nyama ni ukatili uliopotiliza na halitafumbiwa macho na kwa sasa tunaviachia vyombo vya Ulinzi na Usalama viendele na hatua za kisheria," alisema.


Hata hivyo Mkuu wa wilaya huyo alionya tabia ya wananchi kujichukukia sheria mkononi kwa kuwa kufanya husbabisha madhara mbalimbali ikiwemo vifo na kwamba serikali itamchukulia hatua kila atakayebainika kuhusika.


Aliwasihi wananchi kutoa taarifa kwa vyombo vya Dola na serikali ya kijiji kila wanapobaini tatizo lolote ili lishughulikiwe katika njia zilizo sahihi na kwa wakati.Post a Comment

0 Comments