WAZIRI NDEJEMBI AWATAKA WAAJIRI KUWASILISHA MICHANGO YA WATUMISHI KWA WAKATI KATIKA MIFUKO YA HIFADHI YA JAMII

 






Na Isiaka Hamis Kikuwi

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu) Deogratius Ndejembi amesema Serikali haitamvumilia mwajiri ambaye hatawasilisha michango ya watumishi kwenye Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kwa wakati.

Ametoa kauli hiyo leo Mei 14, 2024 jijini Dar es Salaam akizungumza na waandishi wa habari baada ya kufanya zaira katika ofizi ya Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) Makao Makuu na kuzungumza na Menejimenti ya taasisi hiyo.

"Kuna michango ambayo inacheleweshwa kuletwa, unakuta mwajiri anakata mchango ule kwa mwajiriwa kwa ajili ya kuleta huku katika Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, lakini hailetwi kwa wakati, na mwajiriwa yule anapofika aidha amestaafu ama utumishi wake umekoma kwasababu moja ama nyingine anaanza kuja huku kwenye Mifuko anakuta kwamba mchango wake haukuletwa. Sasa hatutowavumilia waajiri wowote wale ambao watamkata mtumishi wake fedha, lakini fedha hiyo haitawasilishwa kwenye mfuko wa hifadhi ya jamii," amesema Ndejembi na kuongeza,

"Wapo waajiri ambao tumeona wanafanya hivyo, sasa ile ni kumyima haki mwajiriwa katika eneo la kazi la kuweza kupata fedha yake, na kuna waajiri wengine, anakata fedha ya kwake, anakata fedha ya mwajiriwa na anatakiwa alete mchango wake yeye kama mwajiri, lakini anaoufikisha kwenye Mfuko wa NSSF ni ule aliomkata mwajiriwa peke yake. Lakini ule mchango wake yeye anaotakiwa kuuleta nao haufikishi. Mwisho wa siku unakuta mtu akistaafu anaanza kuzungushwa kupata michango yake anahisi ni Mfuko unaomzungusha, lakini kumbe Mwajiri wake hakuleta ile michango. Sasa tutakuwa wakali sana kwa watu wote ambao hawaleti michango yao kwa wakati, ni kwa mujibu wa sheria, iliyoanzisha mifuko hii ya jamii kuhakikisha kwamba waajiri wanaleta michango kwa wakati. Kwahiyo tutasimamia hili kwa ukali kwelikweli,".

Akizungumzia kuhusu NSSF, Waziri Ndejembi amesema kuwa Mfuko huo umekuwa ukifanya kazi vizuri na kwamba chini ya uongozi wa Mkurugenzi Mkuu Masha Mshomba imeshuhudiwa kasi ya ukuaji wake. 

Kwamba Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alipoingingia madarakani mwaka 2021 na Kumteua Shomba kuwa Mkurugenzi Mkuu, Mfuko ulikuwa na thamani ya shilingi Trilioni 4.8, lakini ndani ya miaka mitatu ukuaji wa Mfuko umefikia thamani ya shilingi Trilioni 8.1.

"Huu ni ukuaji wa hali ya juu, na nimafanikio makubwa kwa Serikali ya Awamu ya Sita, ni mafanikio makubwa yaliyoletwa na Mkurugenzi wa Taasisi hii na Menejimenti yake kwa ujumla. Lakini ukiacha mafanikio haya kuna mambo ya msingi ambayo ni lazima tuyaone yakitokea," amebainisha Ndejembi.
Kwamba wanataka kuona Mfuko unaongeza nguvu ya huduma kwa mteja ambaye ni Mtanzania yule ambaye anachangia kwenye Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, kwa kuhakikisha wanahudumiwa kwa wakati, na kwere zao zozote ambazo wanaleta ziweze kuchukuliwa hatua mara moja," amesema Ndejembi na kubainisha,

"Lakini pia katika hilo wao (Menejimenti ya NSSF) wameweza kunieleza kuwa kama Menejimenti wameweza kuchukua hatua kubwa za kujenga mifumo ya TEHEMA ya kuhakikisha mteja anapata huduma kwa haraka. Jinginea ambalo tumesisitiza ni kuhakikisha kwamba fedha hizi za Watanzania ambazo zipo kwenye Mifuko ya Hifadhi ya jamii iwekezwe vizuri na kwa uadilifu wa hali ya juu, kuwekeza kwenye miradi ambayo itarejesha fedha za watu walizowekeza ili tuweze kulipa mafao kwa wakati. Lakini vilevile miradi hiyo iweze kurejesha fedha na faida zaidi katika mifuko hii," ameeleza Ndejembi.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa NSSF Shomba ameahidi kwamba yote waliyoelekezwa na kusisitizwa na Waziri Ndejembi watayatakeleza ikiwemo suala la kuboresha huduma kwa wateja. Kwamba watahakikisha wanashauriana na wadau wengine ili kufanikisha maboresho hayo.

Kadhalika amesema kuwa watahakikisha wanakuwa na usimamizi mzuri wa miradi wenye tija ambao utarejesha faida na kusaidia kulipa mafao kwa wastaafu.






Post a Comment

0 Comments