ELIMU YAITAJIKA ZAIDI JUU YA KUTOKUWATENGA WAGONJWA WA KIFAFA

 



Na mwandishi wetu

Waratibu wa afya ya Akili na magonjwa yasiyoambukizwa Mkoani Geita wametakiwa kuwa mstari wa mbele kutoa elimu kwa  wananchi juu ya kuachana na dhana ya kuwatenga watu ambao wanamatatizo ya ugonjwa wa kifafa.


Kifafa huchangia sehemu kubwa ya mzigo wa magonjwa duniani, unaoathiri karibu watu milioni 50 duniani kote. Kadirio la idadi ya watu kwa ujumla walio na kifafa hai (yaani, mishtuko ya ubongo inayoendelea au wanaohitaji matibabu) kwa wakati fulani ni kati ya 4 na 10 kwa kila watu 1000.


Ulimwenguni, kila mwaka  takriban watu milioni 5 hugunduliwa kuwa na  kifafa. Katika nchi zenye kipato cha juu, inakadiriwa kuwa watu 49 kati ya 100,000 wanagunduliwa na kifafa kila mwaka. Katika nchi zenye kipato cha chini na cha kati, takwimu hii inaweza kuwa watu 139 kwa kila watu 100 000.


Kufuatia uwepo wa tatizo la ugonjwa huu ambao umekuwa ukisababisha unyanya pakaa kwenye Jamii ,Mganga Mkuu wa Mkoa wa Geita ,Omary Sukari amekutana na waratibu wa afya ya akili na magonjwa yasiyoambukizwa ambapo ametumia nafasi hiyo kuwasisitiza kutoa elimu kwenye jamii juu ya madhara ya kumnyanyapaa mgonjwa mwenye Kifafa.


“Niwaombe sana waratibu twendeni kwenye jamii tukatoe elimu juu ya kuacha kumtenga mgonjwa mwenye tatizo la kifafa lakini ikiwezekana hata kuwaeleza watu ugonjwa huu unasababishwa na nini nini dalili zake tunavyo vyombo vya habari vinafanya vizuri tu hapa Mkoani kwetu tutumie hivi vyombo kutoa elimu kwa jamii na vingine ni bure kabisa na wanavipindi vya afya shida imekuwa kuwapata madaktari na wataalamu wa afya nitoe wito twende tukatoe elimu kwa wananchi”Omary Sukari Mganga Mkuu wa Mkoa wa Geita.


Dkt Sukari ameongeza kuwa Mkoa wa Geita ni moja wapo ya eneo ambalo linawaathirika wengi wa ugonjwa na kwamba endapo watauwahisha ugonjwa wa kifafa ni rahisi kutibika .


Naye mratibu wa afya ya Akili Mkoani Geita Elfredina Felix amesema mafunzo ya ugonjwa wa kifafa yamekuja kwa wakati sahihi kwani sasa wanakwenda kutoa elimu kwa wananchi juu ya namna ya kujikinga na kuwatibu wenye ugonjwa huo.







Post a Comment

0 Comments